Kwa Nini Kuna Makanisa Mengi? Na Dan McVey

Tunatazama kila mahali na kuona kitu gani? Makanisa kila mahali, makanisa mengi tofauti, yote yanafundisha mafundisho tofauti, yote yana majina tofauti, yote yakijaribu kumtumikia Mungu mmoja. Kwa nini? Kwa nini makanisa mengine hufundisha wokovu ni kwa njia ya neema peke yake? Kwa nini mengine yanafundisha wokovu ni kwa njia ya imani peke yake a mengine wokovu ni kwa njia ya matendo?

Tutafundishaje, wote mafundisho tofauti kuhusu njia ya wokovu na wakati huo huo kudai kwamba tumeunganika sote katika Kristo?

Naamini sababu moja ya kuwa na makanisa mengi ni ya kukosa kulifahamu neno la Mungu. Katika Mat. 22:29 Yesu alijibu swali kwa kusema, “Mwapotea kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Watu hufundishwa vitu tofauti na wanaviamini kwa sababu hawaifahamu Biblia na yale yanayofundishwa na Biblia. Hata mtume Paulo alisema, kwamba maisha yake ya dhambi kabla ya kufanyika kuwa Mkristo aliyatenda katika ujinga na kwa kutokuamini, 1 Tim. 1:13. Ujinga siyo kisingizio, Mungu anatutaka tuufahamu ukweli. Yesu alisema, “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Yoh. 8:32. Kwa kuifahamu kweli tutaitii kweli. Ikiwa hatuyafahamu yanayofundishwa katika Biblia, ni rahisi kupotoshwa na mafundisho ya uongo.

Sababu nyingine inayofanya kuwe na makanisa mengi ni ya kwamba kuna watu wengi ambao hawafundishi neno la Mungu inavyostahili. Biblia inatuonya mara nyingi kuhusu walimu wa uongo wanooweza kutuongoza dhambini. “Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwa yamkini hata walio wateule.” Math. 24:24. “Yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake shetani, kwa uwezo wote, na ishara za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea, kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa, kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu,” 2 Thes. 2:9-12. “Basi Roho anena wazi wazi kwamba nyakati za mwisho, wengine watajitenga na imani wakisikiliza Roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani, kwa unafiki wa watu wasemao uongo wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe, wakiwazuia watu wasioe na kuwaamuru wajiepushe na baadhi ya vyakula ambavyo Mungu aliviumba vipokelewe kwa shukurani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli,” 1 Tim. 4:1-3. (Na maandiko mengine mengi.) Biblia inatuonya tutumie kwa halali neno la Mungu (2 Tim. 2:15) hii inamaanisha kwamba neno la Mungu linaweza likatumika katika njia isiyo halali, tusipokuwa waangalifu. Ikiwa mtu anakueleza kuwa yeye ni dereva na umpe gari lako, utakuwa hatarini asipoliendeha vizuri. Anaweza kuliharibu gari lako na pengine kukuua.

Sababu moja kubwa ya kuwa na makanisa mengi ni kwa sababu watu hawaliheshimu neno la Mungu. Tunamheshimu Rais, Baba mzazi, jumbe; lakini Mungu akisema, hatumsikilizi. Kwa hiyo watu wanadharau kile Mungu anachosema na kuamini kile wanachokipenda kuamini. Lakini sikiliza! Biblia inasema tumelaaniwa tukiondoa lo lote katika neno la Mungu na kuongeza cho chote juu ya neno lake, wala hatuna ruhusa kubakilisha kwa njia nyingine yo yote ile. “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya kitabu hiki; mtu ye yote akiongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki,” Ufu. 22:18-19. “Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia,” 2 Yoh. 9. Yesu alisema, “nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu,” Mk. 7:7. Agano Jipya linatuhimiza kujitahidi kuutambua ukweli uliofunuliwa mara moja kwa njia ya Kristo. “Wapenzi nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu,” Yuda. 3.

Wapendwa, kuna makanisa mengi sana duniani lakini Mungu hayafurahii. Makanisa ambayo yanatokana na ujinga, mafundisho ya uongo, kiburi na sababu zingine za kidunia. Yesu aliomba kwamba wanafunzi wake wote wawe na umoja kama vile Yeye ni mmoja. “Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja, kama vile Baba ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh. 17:20-21. Biblia inafundisha kuwa Kristo ana mwili mmoja (Efe. 4:4) ambao ni Kanisa, “Akavitia vitu vyote chini ya miguu yake ili amweke awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe. 1:22-23. Mungu ana Kanisa moja tu. Lakini ulimwenguni kumejaa makanisa mengi, Mungu hayafurahii. Tufanyeje? Tunalazimika kujitahidi kuwa Kanisa tunalolisoma katika Agano Jipya na iwe hivyo tu. Ikiwa wewe ni mmojawapo mwenye kuutafuta ukweli, tunakushauri uvitafakari baadhi ya vikundi vya watu. Sisi tunajitahidi kuwa wakristo peke yake. Tunataka kuifuata Biblia tu. Hatuna makao makuu duniani, hatuna ofisi kuu, hatuna baraza kuu wala dogo, ama kundi la watawala hatuna. Tunaabudu bila kuipamba ibada, kama vile Agano Jipya la Yesu Kristo linavyotuagiza. Tunafundisha kama vile Agano Jipya linavyoamuru kuhusu njia ya wokovu. Tunamtia moyo kila mshirika mwenzetu, kuishi maisha ya utauwa katika uhuru wa imani, akimtumikia Bwana kila siku kwa imani moja ya watu wote.ukitaka kujua mengi yanayotuhusu soma Agano Jipya na kuona jinsi watu wa Mungu wanavyotakiwa kuwa. Tutazame na kujifunza nasi. Tusaidie tunapojitahidi kuurudisha Ukristo wa Agano Jipya. Udhehebu (wingi wa makanisa) umeufanya ulimwengu kukosa imani katika Kristo. Tunatakiwa kuwa watu wa Mungu peke yake na kuyatupilia mbali mafundisho ya wanadamu. Mungu na apewe utukufu sio mwanadamu. Mungu na aongoze imani yetu si mwanadamu. Yesu alisema, “Nitalijenga Kanisa langu,” Mat. 16:18. Lazima tujitahidi kuwa Kanisa hilo kama vile ilivyo katika Agano Jipya. Ikiwa Kristo alilijenga Kanisa lake (na kwa kweli alijenga), tunatakiwa kujitahidi kuwa kanisa hilo moja kwa kufuata neno lake. Tunajua hakuna wokovu nje ya Kristo, “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa, naye ni Mwokozi wa mwili,” Efe. 5:23. “Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele,” 2 Tim. 2:10. Kwa hiyo, ni lazima tujitahidi kuwemo ndani ya Kristo na kuwa watu wake. Kwa nini usije tukashauriana? “Haya njooni, tusemezane asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa. 1:18. Je, unapendezwa na utaratibu wa Agano Jipya? Je, unapendezwa na Ukristo safi? Ninatumaini hivyo. Tafadhali onana nasi, utakuta tunaitwa “Makanisa ya Kristo” kwa sababu ndivyo tunavyojitahidi kuwa-Kanisa la Kristo. Karibu tushikamane pamoja tukijitahidi kuurudisha Ukristo wa Agano Jipya!

KUJUZWA NEEMA YA MUNGU

Mtu asomapo aya zifuatazo za maandiko mara huona tatizo la dhambi linadhihirika katika maisha yake (Isaya 59:1-2; 64:6: Warumi 3:10, 23). Tunapozungumzia dhambi, kimsingi tunakuwa tunazungumzia ile ambayo humaanisha “kukosea” 1 Yohana 3:4; 5:17). Imesemwa kwamba “ingawaje wanadamu wanatofoutiana kwa kiasi kikubwa katika asili na ukubwa wa hali ya utenda dhambi, katika ukweli kwamba wote wametenda dhambi, hakuna tofauti kabisa baina ya watu bora na duni”. Pia imesemwa kwamba “Neema ya Mungu haimfai yeyote anayeshindwa kuona uhalisia na ukubwa wa udhalimu wa dhambi za mwanadamu.

Kwa kweli, peke yetu, tunasimama katika hali ya kuhukumiwa mbele za Mungu. Wakati fulani tunaimba, “Nasimama huku nashangaa mbele za Yesu Mnazareti, na nastaajabu jinsi gani angeweza kunipenda, mwenye dhambi niliye hukumiwa kuwa najisi” Bila Kristo tunastahili kutengwa na Mungu milele yote linapokuja suala rahisi la haki.

Kwa urahisi fanya hivi, endapo tunataka kuielewa neema ya Mungu, lazima tuielewe adhabu ambayo ingekuwapo bila neema. Katika makala hii, tunataka kujijuza juu ya neema ya Mungu.

NEEMA YA MUNGU INAVYOFAFANULIWA

Msingi wa neno “charis”, ambalo ndilo lililotafsiriwa neema, lina vipengele vingi ambavyo hutusaidia kukubali kazi ya neema. Katika maandishi ya Kiyunani cha kale, neno hili humaanisha kile “kilichotolewa kwa hiari, kwa kupenda au kufuatana na upendeleo”. Lilitumika pia katika mazingira ya matamshi yenye kujenga na kuinua. Kwa mfano, zingatia maneno ya Paulo katika Waefeso 4:29. Mahali penginepo neno hili kwa kiyunani lililotafsiriwa neema humaanisha, “Urafiki uliovunjika unaopelekea tendo la ukarimu,huruma, ukarimu wa upendano, kutakiana heri kiujumla” (Luka 2:52. Pia linamaanisha hali ya shukrani anayokuwa nayo mtu angeihisi kutokana na matendo ya upendeleo ambayo angeyapata. Pia tunatakiwa tuzingatie kuwa fafanuzi zote zinajikita kwamba neema ni kitu chema ajabu, kwa mpokeaji peke yake.

Katika mazingira ya kiroho kuhusiana na neema ya Mungu, neema humaanisha “isiyotokana na matendo, upendeleo wa Mungu ambao hustahili. “Katika Warumi 6:23 maneno “karama” yametokana na neno la Kiyunani “charisma” ambalo kwalo twapata “charismatic” neno ambalo kimsingi humaanisha “karama ya neema” au “karama isiyotokana na matendo”. Pia katika Tito 3:5 twaweza kuona maneno ya Paulo. Ni muhimu kutambua kuwa neema tele na huruma tulizoshushiwa ni kwa sababu “Mungu ni pendo” (1 Yohana 4:8).

UAMUZI WA MUNGU

Ni vigumu kuelewa kina cha upendo, neema na huruma za Mungu (Waefeso 3:17-19). Katika kilindi cha kina cha pendo lake, ulifanyika uamuzi wa kumtuma Kristo kabla ya “misingi ya ulimwengu” (Waefeso 1:4). Kwa uzuri wa pendo lake aliamua kumtuma “mwanawe wa pekee” Yohana 3:16). Vile vile tunatambua upendo wa Uungu, kama ulivyoonekana katika uamuzi wa Kristo kufanya kila lililowezekana ili kuwakomboa wanadamu (Yohana 1:1,2; 17:5; Wafilipi 2:6,7). “Alijidhalilisha” kama kiyunani kinavyoonyesha, “alijifanya mtupu”. Hii hutoa umbali kiasi gani Yesu alienda ili kutupa nafasi ya kuokolewa kwa neema yake.

NEEMA YA MUNGU IMEDHIHIRISHWA

Mwana wa Mungu alipokuja katika ulimwengu huu alitolewa msalabani kama “mbadala” wa dhambi zetu (1 Yohana 2:1, 2). Hili linaweza lisilete maana sana kwetu hadi tutakapoelewa kuwa “mbadala” humaanisha “upatanisho” au “kufa kwa ajili ya kupatanisha” hali inayomaanisha kukarabati, kufidia.” Neno hili linamaanisha kuigeuza ghadhabu.

Haki ya Mungu hudai uwepo wa malipo ya dhambi; ambayo Yesu alitulipia. Mwanzoni wa makala hii tuliona kwamba dhambi zetu hututenga na Mungu (Isaya 59:1-2); matokeo yake tumetengana na Mungu, tuko katika faraka. Kwa sababu ya hili, kinachohitajika ni usuluhishi. Usuluhishi ni “kuufanya upya uhusiano wa karibu”. Katika kujifunza Agano Jipya twaona ya kuwa Yesu alijitolea kuwa sadaka sadaka mbadala (2 Wakorintho 5:21). Katika aya hiyo hiyo ya 2 Wakorintho 5, Paulo alionyesha kuwa walikuwa wamepewa “huduma ya upatanisho,” iliyotoa ufahamu wa kuwezesha kupokea matendo ya neema ya Mungu (2Wakorintho 5:18).

Katika dhabihu yake ya ajabu, Kristo anatuwezesha kupata ukombozi. Katika kitabu chake cha Greek-English Lexicon, Thayer anafafanua neno ukombozi kama “kuachiliwa kunakotokana na malipo ya fidia”. “Bila Yesu sisi ni “watumwa wa dhambi” (Warumi 6:17), na kwa hivyo “tumeuzwa chini ya dhambi” (Warumi 7:14). Kama vile Paulo alivyoeleza katika maandiko yake kwa Tito, Yesu “alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote” (Tito 2:14).

Katika neema ya Mungu, kitu pekee kinachoweza kufikia gharama za ukombozi na kiwezacho kuleta upatanisho ni damu ya Kristo. Petro aliandika kuwa mwanadamu amekombolewa “….kwa damu ya thamani, kama ya mwanakondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo” (1 Petro 1:18, 19). Kuna vitu amabvyo vinaweza kukombolewa kwa fedha na dhahabu, lakini ni damu ya Kristo pekee iwezayo kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye dhambi. Paulo alilidhihirisha hili kwa waefeso alipowambia kuwa kipindi fulani walikuwa “wafu” bila Kristo kwa sababu ya makosa na dhambi. (Waefeso 2:1,12-13)

NEEMA YA MUNGU IMEENEA NA INAPATIKANA

Hili linaonekana katika maneno ya Mtume Paulo katika Tito 2:11. Hata ingawa Kristo alijitoa kuwa dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi za wanadamu wote, haimanishi kwamba kila mtu ataokolewa. Katika Kiyunani, wazo la kuleta wokovu limejikita katika uwezekano na siyo uhalisia. Imesemwa kwamba “kama dawa iko kwenye sanduku, ndani ya chupa yenye kifuniko, mgonjwa hawezi kupona. Hilo siyo tatizo la dawa; ni tiba, lakini hakuna tiba inayoweza kufanya kazi wakati haijatumika. Hivyo, kuenea kwa karama, uwezo wa karama mahali pote, siyo ufinyu wa kiwango cha waliofikiwa kwa sababu eti kule wasikoichukua, basi manufaa yake hayatambulikani.

Ni kweli Mungu anataka watu wote waokolewe (2 Petro 3:9); walakini, katika hekima ya Mungu isiyo ukomo, Uumbaji wa Mungu ulikuwa kwamba mwanadamu awe na utashi. Twaweza kulifafanua hivi; Chukulia Mungu kwa mikono iliyoonyooshwa ameshika zawadi ya thamani kubwa; zawadi ambayo hustahili lakini unapewa bure.. Hata ingawa inatolewa bure, kwa namna yoyote hustahili kuipata. Imekufikia, lakini kuna masharti yaliyowekwa ili uipate. Unatakiwa uamue kama unaitaka ile zawadi ama la. Mungu anaweka wazi kwamba neema yake inapatikana kwa wale walio tayari kutii mapenzi yake (Mathayo 7:21; Waebrania 5:8, 9). Ingawaje ni zawadi ambayo hatuitolei jasho, hatuwezi kuokolewa mpaka tukidhi mashariti ya Mungu. Kwa hali hiyo, Mungu ametuletea neema yake sasa. Uamuzi ni wetu (Mathayo 6:24)

‘KUAMINI’ MAANA YAKE NINI?

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu,hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe nauzima wa milele” Yohana 3:16. Mstari huu ni moja ya mistari inayopendwa katika Biblia, na bado ni moja ya mistari ya Biblia iliyokosewa kueleweka. Sintofahamu hiyo hutokana na watu kuchanganya maana ya “kuamini”. Wengine hufundisha kuwa neno “amini” hapa humaanisha tu kumtambua Yesu kama mwokozi, na kwamba endapo wakifanya hivyo wanakuwa kwenye hali ya kuokolewa.

Neno “amini” katika Yohana 3:16 hutokana na neno la Kiyunani pisteuo, linalomaanisha ushawishi, tumaini la furaha, muunganiko wa utiifu. Neno “amini” katika Agano Jipya mara nyingi hubeba dhana ya utii. Neno hili pekee yake halimaanishi “saini ya kifikra.”

Mtu anaweza kutazama mazingira ambayo waziwazi Yohana 3:16 huangukia na ataweza kuona ushahidi kwamba katika mstari huu Yesu alimaanisha mambo mengi zaidi ya saini ya kifikra.  Mazingira yenyewe ni Yohana 3:1-21. Na katika mistari hii twajifunza mambo matatu ambayo nataka kuyazingatia:

  1. Ili mtu awe ndani ya Yesu, ni lazima azaliwe mara ya pili, kuzaliwa kwa maji na kwa roho, Yohana 3:1-8.
  2. Katika Yohana 3:14 kuna nukuu ya Musa kumwinua nyoka jangwani. Hata kale, waliomtenda Mungu dhambi, hawakukaa tu nyumbani huku wakiamini kuwa yule nyoka wa shaba angewaokoa. Kimsingi walitakiwa kuinuka, kutembea kutoka hemani mwao, ambapo yawezekana ilikuwa ni umbali wa maili kadhaa (kumbuka kulikuwa na kambi ya watu wapatao milioni tatu) ili kufika mahali palipokuwa na yoka wa shaba ili kumtazama ili wawe hai, Hesabu 21:9. Ni wazi kwamba katika wokovu wao kulikuwa na zaidi ya saini ya kifikra

3) Yesu alidhihirisha kwamba endapo unataka kuijia nuru, kulikuwa na jambo ambalo mtu ulitakiwa kulifanya, “Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru,” Yohana 3:21.

Tuelewe kutokana na Neno la Mungu kuwa imani ya Kibiblia huhusisha imani inayompelekea mtu kutumaini na kutii. Kushindwa kutumaini na kumtii Yesu ni kushindwa dhahiri kumpokea kama Bwana na mwokozi. “Na kwanini mwaniita Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?” Luka 6:46

Kunyunyizia, Kumwagia, Au Kuzamisha – Ni Upi?

I. UBATIZO WA MAJI UMEAMRIWA.

a. Mt. 28:19, “Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.”

b. Mdo. 2:38, “Petro akawaambia, tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu….”

c. Mdo 10:48, “Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo.”

d. Mdo. 18:8, “..na Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.”

e. Mdo. 22:16, “Basi, sasa unakawilia nini? Simama ubatizwe ukaoshwe dhambi zako..”

f. Rum. 6:3, “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika kristo yesu tulibatizwa katika mauti yake.”

g. Hapa tumekwisha kuona jinsi Kristo na mitume walivyoamuru ubatizo kama ni kanuni ya wokovu (au ondoleo la dhambi) na kwa kuongozwa na Kristo.

II. NI AKINA NANI WANAOHUSIKA KUBATIZWA?

a. Ni wale wanaoweza kufundishwa, Mt. 28:18-20.

b. Ni wale wanaoamini, Mk. 16:15-16.

c. Ni wale waliotubu, Mdo. 2:38.

d. Ni wale waliomkiri, Mdo. 8:37. “Filipo akasema, ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana akajibu, akanena, naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.”

e. Watoto wadogo sio somo la ubatizo.  Hawajapotea; mtu hawezi kuokolewa kama hajapotea. Watoto wadogo hawajapotea wako salama hawana dhambi, Eze.18:20.  Pia, Watoto wadogo hawawezi kuamini, kutubu, au kumkiri Kristo, Mdo. 2:37.

III. WENGINE WALIBATIZWA TENA KATIKA AGANO JIPYA?

a. Paulo aliwakuta watu waliobatizwa ubatizo wa Yohana kabla ya sheria za Kristo kukamilika, Mdo. 19:3.

b. Kwa mafundisho ya Paulo, waliona inawalazimu kubatizwa tena kwa jina la Bwana Yesu; na kwa madhumuni aliyoyaeleza Kristo.

c. Wengi siku hizi wamebatizwa kwa njia isiyo sawa au kwa madhumuni yasiyo sawa; hawa wanapaswa kubatizwa kwa ondoleo la dhambi, Mdo. 2:38; Rum. 6:1-11.

IV. KUNYUNYIZIA, KUMWAGIA AU KUZAMISHA NI UPI?

a. Ubatizo ni kuzika: “Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu,” Kol. 2:12.

b. Ubatizo unahitajika. 1) Maji mengi, Yoh. 3:23. 2) Ni kutelemka majini, Mdo. 8:38. 3) Ni kuzama ndani ya maji, Mdo. 8:38. 4) Ni kupanda toka majini, Mt. 3:16. Yesu alibatizwa (kuzamishwa) na Yohana, si kwa ondoleo la dhambi, lakini ni kwa kuitimiza haki yote. Kwani Yeye hakuwa na dhambi.

c. Katika neno la Mungu “Ubatizo.”  1) “Ubatizo” tafsiri ya Kiyunani katika Agano Jipya ni baptizo. Neno hili linaeleza maana yake ni kutumbukiza, ni kuzamisha, na kadhalika.” 2) “Kunyunyiza” tafsiri ya Kiyunani katika Agano Jipya ni “Rantizo;” na kumwagia ni “Cheo”. 3) Mahali popote ambapo neno “ubatizo” linaonekana au kusemwa au kuandikwa ni baptizo sio rantizo au cheo.

V. Historia ya Affusio kunyunyizia au kumwagia (Kanisa lilianza mwaka 33 B.K.).

a. Mageuzi haya yaliandikwa mnamo 251 B.K. alipokuwa amelala kitandani kwa ajili ya ugonjwa.

b. Hapo kwanza, Affusio ilikuwa ikubaliwe na watawala kwa udhaifu.

c. Baraza la Ravenna, wakati wa 1311 B.K. liliutambua ubatizo wa kunyunyiza katika kanisa Katoliki.

d. Affusio ni uzushi wa wanadamu, ambao hauwezi kutimiza mpango wa Mungu wa wokovu.

VI. Kusudi la Ubatizo wa Agano Jipya.

a. “Unawaokoa ninyi pia siku hizi,” 1 Pet. 3:20-21.

b. Na matokeo yake ni msamaha wa dhambi, Mdo. 2:38.

c. “Unasafisha dhambi,” Mdo. 22:16.

d. “Unatuweka ndani ya Kristo,” Gal. 3:36-27.

e. Tulibatizwa “katika mauti ya Kristo,” Rum. 6:3-4. Kristo alimwaga damu kwa mauti yake, Yoh. 19:32-37. Tulibatizwa katika mauti yake. Ni katika ubatizo unaposhiriki damu ambayo husafisha dhambi zetu.

http://www.kanisalakristo.com