Kwa Nini Kuna Makanisa Mengi? Na Dan McVey

Tunatazama kila mahali na kuona kitu gani? Makanisa kila mahali, makanisa mengi tofauti, yote yanafundisha mafundisho tofauti, yote yana majina tofauti, yote yakijaribu kumtumikia Mungu mmoja. Kwa nini? Kwa nini makanisa mengine hufundisha wokovu ni kwa njia ya neema peke yake? Kwa nini mengine yanafundisha wokovu ni kwa njia ya imani peke yake a mengine wokovu ni kwa njia ya matendo?

Tutafundishaje, wote mafundisho tofauti kuhusu njia ya wokovu na wakati huo huo kudai kwamba tumeunganika sote katika Kristo?

Naamini sababu moja ya kuwa na makanisa mengi ni ya kukosa kulifahamu neno la Mungu. Katika Mat. 22:29 Yesu alijibu swali kwa kusema, “Mwapotea kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Watu hufundishwa vitu tofauti na wanaviamini kwa sababu hawaifahamu Biblia na yale yanayofundishwa na Biblia. Hata mtume Paulo alisema, kwamba maisha yake ya dhambi kabla ya kufanyika kuwa Mkristo aliyatenda katika ujinga na kwa kutokuamini, 1 Tim. 1:13. Ujinga siyo kisingizio, Mungu anatutaka tuufahamu ukweli. Yesu alisema, “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Yoh. 8:32. Kwa kuifahamu kweli tutaitii kweli. Ikiwa hatuyafahamu yanayofundishwa katika Biblia, ni rahisi kupotoshwa na mafundisho ya uongo.

Sababu nyingine inayofanya kuwe na makanisa mengi ni ya kwamba kuna watu wengi ambao hawafundishi neno la Mungu inavyostahili. Biblia inatuonya mara nyingi kuhusu walimu wa uongo wanooweza kutuongoza dhambini. “Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwa yamkini hata walio wateule.” Math. 24:24. “Yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake shetani, kwa uwezo wote, na ishara za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea, kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa, kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu,” 2 Thes. 2:9-12. “Basi Roho anena wazi wazi kwamba nyakati za mwisho, wengine watajitenga na imani wakisikiliza Roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani, kwa unafiki wa watu wasemao uongo wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe, wakiwazuia watu wasioe na kuwaamuru wajiepushe na baadhi ya vyakula ambavyo Mungu aliviumba vipokelewe kwa shukurani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli,” 1 Tim. 4:1-3. (Na maandiko mengine mengi.) Biblia inatuonya tutumie kwa halali neno la Mungu (2 Tim. 2:15) hii inamaanisha kwamba neno la Mungu linaweza likatumika katika njia isiyo halali, tusipokuwa waangalifu. Ikiwa mtu anakueleza kuwa yeye ni dereva na umpe gari lako, utakuwa hatarini asipoliendeha vizuri. Anaweza kuliharibu gari lako na pengine kukuua.

Sababu moja kubwa ya kuwa na makanisa mengi ni kwa sababu watu hawaliheshimu neno la Mungu. Tunamheshimu Rais, Baba mzazi, jumbe; lakini Mungu akisema, hatumsikilizi. Kwa hiyo watu wanadharau kile Mungu anachosema na kuamini kile wanachokipenda kuamini. Lakini sikiliza! Biblia inasema tumelaaniwa tukiondoa lo lote katika neno la Mungu na kuongeza cho chote juu ya neno lake, wala hatuna ruhusa kubakilisha kwa njia nyingine yo yote ile. “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya kitabu hiki; mtu ye yote akiongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki,” Ufu. 22:18-19. “Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia,” 2 Yoh. 9. Yesu alisema, “nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu,” Mk. 7:7. Agano Jipya linatuhimiza kujitahidi kuutambua ukweli uliofunuliwa mara moja kwa njia ya Kristo. “Wapenzi nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu,” Yuda. 3.

Wapendwa, kuna makanisa mengi sana duniani lakini Mungu hayafurahii. Makanisa ambayo yanatokana na ujinga, mafundisho ya uongo, kiburi na sababu zingine za kidunia. Yesu aliomba kwamba wanafunzi wake wote wawe na umoja kama vile Yeye ni mmoja. “Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja, kama vile Baba ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh. 17:20-21. Biblia inafundisha kuwa Kristo ana mwili mmoja (Efe. 4:4) ambao ni Kanisa, “Akavitia vitu vyote chini ya miguu yake ili amweke awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe. 1:22-23. Mungu ana Kanisa moja tu. Lakini ulimwenguni kumejaa makanisa mengi, Mungu hayafurahii. Tufanyeje? Tunalazimika kujitahidi kuwa Kanisa tunalolisoma katika Agano Jipya na iwe hivyo tu. Ikiwa wewe ni mmojawapo mwenye kuutafuta ukweli, tunakushauri uvitafakari baadhi ya vikundi vya watu. Sisi tunajitahidi kuwa wakristo peke yake. Tunataka kuifuata Biblia tu. Hatuna makao makuu duniani, hatuna ofisi kuu, hatuna baraza kuu wala dogo, ama kundi la watawala hatuna. Tunaabudu bila kuipamba ibada, kama vile Agano Jipya la Yesu Kristo linavyotuagiza. Tunafundisha kama vile Agano Jipya linavyoamuru kuhusu njia ya wokovu. Tunamtia moyo kila mshirika mwenzetu, kuishi maisha ya utauwa katika uhuru wa imani, akimtumikia Bwana kila siku kwa imani moja ya watu wote.ukitaka kujua mengi yanayotuhusu soma Agano Jipya na kuona jinsi watu wa Mungu wanavyotakiwa kuwa. Tutazame na kujifunza nasi. Tusaidie tunapojitahidi kuurudisha Ukristo wa Agano Jipya. Udhehebu (wingi wa makanisa) umeufanya ulimwengu kukosa imani katika Kristo. Tunatakiwa kuwa watu wa Mungu peke yake na kuyatupilia mbali mafundisho ya wanadamu. Mungu na apewe utukufu sio mwanadamu. Mungu na aongoze imani yetu si mwanadamu. Yesu alisema, “Nitalijenga Kanisa langu,” Mat. 16:18. Lazima tujitahidi kuwa Kanisa hilo kama vile ilivyo katika Agano Jipya. Ikiwa Kristo alilijenga Kanisa lake (na kwa kweli alijenga), tunatakiwa kujitahidi kuwa kanisa hilo moja kwa kufuata neno lake. Tunajua hakuna wokovu nje ya Kristo, “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa, naye ni Mwokozi wa mwili,” Efe. 5:23. “Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele,” 2 Tim. 2:10. Kwa hiyo, ni lazima tujitahidi kuwemo ndani ya Kristo na kuwa watu wake. Kwa nini usije tukashauriana? “Haya njooni, tusemezane asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa. 1:18. Je, unapendezwa na utaratibu wa Agano Jipya? Je, unapendezwa na Ukristo safi? Ninatumaini hivyo. Tafadhali onana nasi, utakuta tunaitwa “Makanisa ya Kristo” kwa sababu ndivyo tunavyojitahidi kuwa-Kanisa la Kristo. Karibu tushikamane pamoja tukijitahidi kuurudisha Ukristo wa Agano Jipya!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s